Friday, July 17, 2015

Banza Stone afariki dunia

Muimbaji wa muziki wa dansi aliyewahi kutamba akiwa na bendi mbalimbali zikiwemo Twanga Pepeta na TOT Band, Ramadhan Masanja maarufu kama Banza Stone amefariki dunia mchana wa Ijumaa, July 17.

banza



Banza alikuwa amelazwa kwenye hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Taarifa kuhusu kifo chake zimethibitishwa na kaka yake pamoja na mmiliki wa Twanga Pepeta, Asha Baraka. Kwa mujibu wa kaka yake, Jabir Masanja, msanii huyo alikuwa anasumbuliwa na fangasi kichwani mwake na dawa alizokuwa anatumia zilikuwa kali kiasi cha kumpotezea hamu ya kula.
Hivi karibuni mama yake mzazi aliongea na kituo cha redio cha EFM na kukiambia kuwa afya ya mwanae ilizidi kuzorota na alianza kugoma kula chakula wala kunywa kunywa dawa. Mama huyo alisema hadi siku hiyo Banza alikuwa amegoma kula kwa siku tatu mfululizo. AliongeZa kuwa pamoja na kuugua hivyo bado wasanii wenzake walishindwa kwenda kumjulia hali.
“Mpaka sasa sijamuona mtu yeyote aliyekuja kumshughulikia na kumwangalia, wamemwacha hivi hivi. Na mimi siwezi kuwalaumu kwanini hamjaja kumwangalia, kila mtu na moyo wake, mwenye kuja atakuja, mimi ntahangaika na mtoto wangu mpaka pale atakapoamua mwenyezi Mungu,” alisema Mama Banza.
Kabla ya hapo muimbaji huyo alizushiwa kufariki mara nyingi. Wiki chache zilizopita Banza alimongea na kipindi cha Leo Tena cha Clouds FM kukanusha.
Ndio naumwa kichwa kina nisumbua sana lakini sasa hivi naendelea vizuri yaani hizo habari za kuzushiwa kifo naona sasa hivi kwangu sijui hata itakuwa mara ya ngapi, maana nimeshazushiwa sana. Mimi mzima na huyo anayeeneza azunguke na mikoa mingine aeneze vizuri,” alisema Banza.
Lakini mimi nipo nyumbani hapa Sinza kwa Mama yangu sasa hivi hapa napata juice yaani marehumu anaongea; aliongeza Banza kwa kicheko.
Inshallah nikiwa vizuri mashabiki wangu wataniona tu lakini nipo mzima.
Mungu ailaze mahali pema peponi. Amen.






No comments:

Post a Comment